Chama cha ACT Wazalendo kimesema kinapigania kuongoza serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar ili kutengeneza mustakabali wa Zanzibar inayohitajika na kuirejesha mahala pake.
Hayo yameelezwa Julai 09,2023 na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hiko @IsmailJussa wakati akitoa mada kwenye kongamano maalum la Vijana Zanzibar lililopewa jina la ‘Mimi na Zanzibar, Zanzibar na Mimi’, kongamano lililofanyika Hotel ya Golden Tilip Airport, ambapo Jussa amesema Wanzanzibar hawahitaji na hawako tayari kuwa na Rais anayewafanya vijana kuwa tegemezi wakati yeye akijilimbikizia mali.
Ameeleza kuwa Rais kabla hajaingia ofisini anaanza kula kiapo cha kuilinda katiba, hivyo wananchi wanatarajia kuona yale anayoyasema wakati wa kiapo anayasimamia na kuyaonesha kwa vitendo wakati wa uongozi wake jambo ambalo amedai kuwa viongozi wanaotokana na Chama cha Mapinduzi (CCM) wameshindwa kusimamia hilo kwa kipindi chote walichoongoza visiwa hivyo.
Katika hatua nyingine Jussa amesema, chama hiko kinahitaji katiba mpya ya Zanzibar itakayoonesha mamlaka kwa Wazanzibar wenyewe
“…tunataka Rais wetu akiondoka tumkumbuke kuwa alijenga na kuiacha Zanzibar kama Taifa la kidemokrasia ambalo linajali utu wa watu wake, na kwamba watu wenyewe ndio ambao wanaochagua na kuwaweka madarakani viongozi wanaowataka”