Na Josea Sinkala, Songwe.
Jeshi la Polisi Mkoani Songwe limekemea kuendelea kushamiri kwa matukio ya uhalifu ikiwemo mauaji na vitendo vya ukatili wa kijinsia hivyo kuitolea mwito jamii kushirikiana na Polisi kuhakikisha wanatokomeza matukio hayo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe ACP Theopista Mallya amefanya kikao na mapadri wa Kanisa Katoliki Mkoa wa Songwe kilichofanyika katika ukumbi wa Kanisa Katoliki-Mlowo wakiongozwa na Father Godfrey Mwasekanga ambaye ni Makamu wa Askofu Mkuu Jimbo kuu la Mbeya.
Akizungumza kwenye kikao hicho Kamanda wa Polisi mkwoa wa Songwe ACP Theoposta Mallya amesema kumekuwa wimbi kubwa la uhalifu mkoani Songwe hivyo Viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kusaidia kutokomeza uhalifu kwa kutoa elimu kwa waumini wao kila wanapokutana kuchukia uhalifu.
Pia katika kikao hicho Kamanda wa polisi Songwe ACP Mallya amezungumzia suala la Mmomonyoko wa Maadili katika jamii ikiwemo katika Jeshi la Polisi ambako kumekuwa kukisikika harufu za kutoa na kupokea Rushwa.
Kamanda Mallya ameeleza kuwa ni haki ya mwananchi kupata dhamana pasipo kutoa pesa au kitu chochote.
Kuhusu suala la utoaji taarifa kwa Jeshi la Polisi ameitaka jamii wakiwemo viongozi wa dini na viongozi wa vijiji na kata kuendelea kutoa taarifa za uhakifu na wahalifu wa aina mbalimbali ikiwemo vitendo vya Wizi, Ukatili, Ujambazi, Mauaji pamoja na ndoa za jinsi moja.
Akihitimisha kikao hicho kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe ameiasa jamii kujitoa kwa dhati kulinda watoto wao badala ya kujikita kwenye shughuli zao muda wote hali inayohatarisha ulinzi kwa mtoto na kujikuta baadhi ya watoto wakifanyiwa vitendo vya Ulawiti na kuwaomba viongozi wa dini waendelee kutoa elimu katika nyumba zao za ibada ili kuthibiti vitendo visivyofaa huku baadhi vikihusishwa na imani potofu za kishirikina.
Kwa upande wake Father Godfrey Mwasekanga amemshukuru Mkuu huyo wa polisi kwa kuwa na moyo wa upendo kwa jamii anayoitumikia na kuendelea kuifikia na kutoa elimu ya kupinga kwa matendo maovu na kuahidi viongozi wa dini kuendelea kushirikiana na serikali kuelimisha wananchi ili kukataa mambo ya uhalifu na yanayokinzana na tamaduni za kiafrika ikiwemo masuala ya ndoa za jinsi moja anayosema ni chukizo kwa Mungu.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe ACP Theopista Mallya amekuwa na desturi ya kutembelea maeneo mbalimbali ya nyumba za ibada katika mkoa wake wa Songwe na kukutana na waumini na viongozi wa dini akitoa elimu ya utendaji kazi wa jeshi la Polisi na wajibu wa wananchi kushirikiana na viongozi kwenye maeneo yao na Polisi ambacho ni chombo chenye wajibu wa kulinda raia na mali zao na kuhakikisha kwa pamoja wanapunguza na kukomesha kabisa matukio ya uhalifu na wahalifu katika kudumisha amani na ustawi wa jamii na kuchochea Maendeleo.