Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza limefanikiwa kukamata watuhumiwa 264 wa makosa mbalimbali ya uhalifu katika kipindi cha siku 13 na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ili kuendelea kuimarisha hali ya ulinzi na usalama katika mkoa huo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza Wilbrod Mutafungwa amesema katika msako huo walifanikiwa kuwakamata watu wawili katika Wilaya ya Magu wakiwa na mafuta ya dieseli lita 160 yadhaniwayo kuwa ni mali ya wizi mapipa 4 matupu ya lita 200,madumu 40 matupu,mpirawa kunyonyea mafuta na ndoo 18 za milimita 18.
“Tumefanikiwa kudhibiti Matukio ya ajali barabarani kwa kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria madereva 13 waliovunja sheria za usalama barabarani, ambapo makosa ya ajali yaliyoripotiwa ni 2, idadi ya watu waliofariki kutokana na ajali 2, majeruhi 3″_Wilbrod Mutafungwa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mwanza
Kamanda Mutafungwa amesema, mafanikio hayo yote yametokana na elimu inayoendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali ya watumiaji wa barabara ambapo kupitia radio, mitandao ya kijamii, magazeti na television hivyo wananchi wameendelea kuelimishwa juu ya masuala mbalimbali ya usalama barabarani.
Aidha Kamanda Mutafungwa akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo amesema, kupitia mpango mkakati ambao Jeshi hilo liliuandaa kwa kushirikiana na jamii katika hali ya kutanzua na kuzuia vitendo vya kihalifu limefanikiwa kutoa elimu kwa jamii jinsi ya kuzuia na kupambana na uhalifu katika maeneo mbalimbali.
Mutafungwa anasema Jeshi hilo linaendelea kutoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili ziweze kufanyiwa kazi kwa wepesi na haraka.