NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, imeahirisha kutoa hukumu ya kesi ya kikatiba ya kupinga mkataba wa Bandari baada ya Mwenyekiti wa jopo la majaji kupata dharula hadi Agosti 10, 2023.
Kesi hiyo ya kikatiba imeahirishwa jumatatu hii na Naibu Msajili wa Mahakama kuu Projestus Kahyoza.
Naibu msajili Kahyoza amesema Mwenyekiti wa jopo la majaji watatu waliosikiliza kesi hiyo amepata dharula (hayupo) hivyo majaji wamepanga kutoa hukumu hiyo Agosti 10, 2023.
Nje ya ukumbi wa mahakama, Wakili Boniface Mwabukusi mmoja wa mawakili wa waleta maombi ameipongeza Mahakama kwa kuandaa mazingira mazuri kwneye usomwaji shauri hilo hasa ukumbi mwingine wa Mahakama ambao wananchi waliofika Mahakamani wangesikiliza kesi kwa njia ya mtandao.
Jumatatu hii viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa hasa Chadema na viongozi wa kidini walifika mahakamani kufuatilia hukumu ya kesi hiyo ya kikatiba kesi ambayo inaonekana kuwa na mguso kwa watu wengi tangu kuanza kwake.
Rose John Mayemba ni mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Njombe ambaye amesema kitendo cha Serikali kuruhusu mtakaba huo wenye matatizo mbalimbali ni sawa na kuruhusu raslimali za nchi kumilikiwa na wageni.
Shauri la kikatiba namba 05/2023 waleta maombi ni Alfonce Lusako na wenzake watatu wakiwakikishwa mahakamani na wakili Mpale Mpoki na wenzake watatu ambao wanapinga mkataba wa Bandari ambao Serikali imeingia na kampuni ya DP World ya falme za kiarabu Dubai wakiainisha mapungufu mbalimbali ya mkataba huo kuwa hauna maslahi kwa Tanzania ambapo wajibu maombi ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa, Katibu mkuu wa wizara ya Uchukuzi, Mwanasheria mkuu wa Serikali na katibu wa Bunge la Tanzania ambao mahakamani wanawakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu Mark Mulwambo na wenzake watatu ambao msimamo wao ni kuwa mkataba huo ni mzuri na wenye nia njema kuiletea Tanzania maendeleo ya kiuchumi.