Serikali imelazimika kutumia Helkopta kutafuta makundi ya wanyama wakali na waharibufu Tembo waliozagaa katika vijiji 25 vya Wilaya ya Same na kuwavisha vifaa maalum vya mawasiliano kufuatilia mwenendo wao miongoni mwa njia za kudhibiti athari za mwingiliano wa shughuli za kibinadamu na uhifadhi.
Zoezi hilo ni utekelezaji wa agizo la waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Mohammed Mchengera alilotoa hivi karibuni alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika wilaya hiyo ya Same ambapo aliagiza mamlaka ya hifadhi za Taifa TANAPA kupeleka Helkopta katika Wilaya hiyo kusaidia zoezi la kuondoa makundi ya Tendo yaliyozagaa katika maeneo mbalimbali na kuwarejesha katika maeneo ya hifadhi.
Oparesheni hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano baina ya taasisi nne zilizo chini ya wizara ya maliasili na utalii,kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Same na wananchi wenyeji ambao wanasaidia kuainisha maeneo walipo Tembo.
Akizungumzia utekelezaji wa Oparesheni hiyo, Mkuu wa hifadhi ya Taifa Mkomazi, kamishna msaidizi wa uhifadhi Emmanuel Moirana amesema kwa siku ya kwanza jumla ya makundi matano ya Tembo yamerejeshwa hifadhini, mkakati uliopo ni kuendelea na zoezi hilo kuondoa changamoto ya mara kwa mara kuripotiwa makundi ya Tembo kuonekana maeneo ya nje ya hifadhi.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni amepongeza jitihada hizo za wizara uharaka wa kutekeleza ahadi ya kuondoa Tembo hao kwa kuongeza vitendeakazi na rasilimali watu, akisema huenda changamato ikapungua na wananchi kuweza kuendeea na shughuli za uzalishaji.
Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Same walioshiriki katika Oparesheni hiyo wamesema kuna idadi kubwa ya Tembo ambao wametoka kabisa kwenye maeneo ya hifadhi na kufanya makazi ya kudumu kwenye maeneo ya vijiji, hali ambayo imesababisha baadhi yao hasa wakulima mwaka huu kukosa kabisa mazao.