Home KITAIFA GST YAKABIDHI KITABU KINACHOONESHA MADINI YAPATIKANAYO TANZANIA KWA MKOA WA DAR ES...

GST YAKABIDHI KITABU KINACHOONESHA MADINI YAPATIKANAYO TANZANIA KWA MKOA WA DAR ES SALAAM

Kitabu kuongeza ufahamu wa Madini, chavutia Wawekezaji

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imekabidhi Kitabu kwa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Aman Mafuru kinachoonesha Madini yapatikanayo Tanzania ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilolitoa katika Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo (FEMATA) 2023 jijini Mwanza la kusambaza vitabu hivyo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini.

Akipokea vitabu hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mafuru amesema Kitabu hicho kitatumika kama ilivyo kusudiwa na kitasaidia Mkoa huo kujua aina za Madini na sehemu yapatikanayo madini hayo.

“Naomba nichukue fursa hii kuipongeza GST kwa kuja na ubunifu wa kufanya tafiti na kuandaa Kitabu kinachoonesha aina za Madini na sehemu yapatikanayo, naamini Kitabu hiki kitawasaidia wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kujua aina za madini yapatikanayo katika maeneo yao”, amesema Mafuru.

Kwa upande wake, Meneja wa Sehemu ya Jiolojia kutoka GST Maswi Solomon amesema Tanzania imebahatika kuwa na Jiolojia pana yenye sifa ya mchanganyiko wa miamba mingi kuanzia ile ya umri mkubwa hadi ya umri mdogo ambayo imefanya Tanzania kuwa na aina mbalimbali za Madini.

Maswi amesema kutokana na tafiti zilizofanyika katika mikoa mbalimbali nchini, iligundulika kuwa Mkoa wa Dar es Salaam una madini Mkakati ambayo yako kwenye Mchanga Mzito wa Baharini (Heavy Minerals), Madini Muhimu ikiwemo Chumvi, Kaolin na Mawe ya Chokaa pia, kuna Madini Ujenzi kama Mchanga na Udongo Mfinyanzi.

“GST imefanya Utafiti wa awali na kuja na mapendekezo ya Madini Mkakati 31 na Madini Muhimu 11 kwa nchi nzima ambapo Mkoa wa Dar es Salaam una Madini Mkakati ya Mchanga Mzito wa Baharini”, amesema Maswi.

Sambamba na hayo, Maswi ametoa wito kwa wadau wa Sekta ya Madini na wananchi kwa ujumla kujipatia nakala ya Kitabu hicho kinachopatikana katika ofisi za GST ili kuongeza ufahamu na kuvutia Wawekezaji katika maeneo yao.

Jumla ya vitabu saba vimetolewa ambavyo vitasambazwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ofisi za Wakuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ilala, Temeke, Ubungo, Kigamboni na Ofisi ya Katibu Tawaka wa Mkoa.

Previous articleHIFADHI YA TAIFA KITULO KUTANGAZWA KITAIFA NA KIMATAIFA ILI KUVUTIA WATALII NA WAWEKEZAJI
Next articleRASMI MANSPAA YA IRINGA YAFIKIA MAKUBALIANO YA KUINUNUA TIMU YA RUVU SHOOTING,NA KUITWA LIPULI FC

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here