Home KITAIFA GST YAANZA UTAFITI WA JIOLOJIA VISIWANI ZANZIBAR

GST YAANZA UTAFITI WA JIOLOJIA VISIWANI ZANZIBAR

Katika kutekeleza moja ya eneo la mashirikiano kati ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Wizara ya Nishati, Maji na Madini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kufanya tafiti za Jiosayansi visiwani humo, timu ya watalaam kutoka GST imeanza rasmi utafiti wa Jiosayansi ili kuhakikisha kuwa Zanzibar inakuwa na ramani ya Jiosayansi ambayo itawezesha kuweka mipango mahususi ya uendelezaji rasilimali zilizoko chini ya ardhi na mipango ardhi.

Akiwakaribisha wataalam wa GST hii leo Novemba 20, 2023 katika Ofisi za Wizara ya Nishati, Maji na Madini ya Zanzibar, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Joseph John Kilangi amewashukuru watalaam hao na kuwataka kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia uzoefu wao wa masuala ya Jiolojia.

Aidha, Kilangi amewahakikishia wataalam hao usalama na kupata ushirikiano kutoka visiwa vyote vya Unguja na Pemba kwa muda wote watakaokuwa kazini.

Kwa upande wake, mtaalam kutoka GST ambaye pia ni Meneja wa Sehemu ya Jiolojia Maswi Solomon akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa GST ametoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu umuhimu wa ramani ya Jiosayansi katika visiwa vya Zanzibar ambayo haikuwepo.

“mbali na madini ya thamani, mafuta na gesi yaliyozoeleka pia, utafiti huu ni muhimu kuanisha maeneo yenye madini ujenzi na maeneo yenye uwezekano wa kuwa na mashimo hatarishi yaani sinkholes/caves ambayo ni miongoni mwa majanga ya asili ya jiolojia (geohazard) kutokana na visiwa hivi kuwa na miamba yenye hali ya chokaa, maumbo ya miamba yenye kuvutia utalii (geotourism), aina ya miamba muhimu ya kuhifadhi maji, ardhi na taarifa za kemia ya udongo”.

Pia, Maswi amesema kuwa taarifa hizo zinaweza kufungamanishwa na sekta ya utalii, kilimo, afya, ujenzi wa miundombinu, maji, madini, nishati na elimu ili kuendana na Vision ya 2030 ya Madini ni Maisha na Utajiri huku akibainisha matokeo ya utafiti huo yatagusa zaidi sehemu ya maisha ya wakazi wa Zanzibar.

Timu ya wataalam wa GST inatarajia kufanya utafiti wa Jiolojia na Jiokemia katika visiwa vya Unguja na Pemba kwa lengo la kuandaa ramani ya Jiosayansi ya maeneo husika.

Previous articleRC MTWARA: WAANDISHI WA HABARI EPUKENI KUTANGULIZA MASLAHI BINAFSI
Next articleMATUMIZI YA VYOO BORA YAMEONGEZEKA NCHINI TANZANIA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here