SERIKALI na Benki ya Dunia wamekubaliana kuanza haraka utekelezaji wa kazi za ujenzi wa mradi wa uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) awamu ya pili.
Makubaliano hayo yamefikiwa kwenye kikao cha pamoja kilichowakutanisha Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Deo Ndejembi, Mwakilishi Mkazi Benki ya Dunia, John Motton na Mratibu wa miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kutoka Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), Humphrey Kenyenye.
Katika kikao hicho viongozi hao wamekubaliana kuwa kazi ya usanifu yakinifu ikamilike ndani ya muda na mpaka kufikia Novemba mwaka huu wakandaras wawe wamewasilisha kwa ajili ya kuendelea na utaratibu wa kutangaza kazi za ujenzi zianze mara moja.
Pia wamekubaliana na kupitisha maeneo yaliyopendekezwa kwa ajili ya kujengwa madampo ya kisasa katika Mkoa wa Dar es Salaam kwenye Halmashauri za Wilaya ya Ubungo, Kigamboni na Kinondoni.
Viongozi hao walikubaliana pia ili kuwe na udhibiti madhubuti wa taka ngumu ni vyema ikaanzishwa wakala utakaosimamia udhibiti wa taka ngumu kwenye Mkoa huo.