Paulo Lwiva ambaye ni mchungaji wa kanisa la EAGT Mtwango wilayani Njombe ameiomba Serikali kumsaidia kumaliza mgogoro wake dhidi ya familia ya diwani wa kata ya Iwungilo George Muhando akidai wanataka kupoka mashamba yake ambayo amewekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji ikiwemo kupanda matunda ya parachichi zaidi ya 2000 kwenye shamba hilo linalopatikana katika kijiji cha Uliwa mjini Njombe.
Amesema eneo hilo alikabidhiwa na wazazi wake tangu mwaka 2007 walipokosa Nguvu lakini anashangaa kuona familia ya diwani wa kata ya Iwungilo George Muhando kutaka kupora mashamba hayo huku akitishiwa kupoteza sadaka zake endapo akiendelea kushindana na familia hiyo ambapo mpaka sasa familia hiyo imekwisha kata miti 70 ya matunda.
Diwani wa kata ya Iwungilo George Muhando amekana kuwa na mgogoro na mwananchi yeyote katika kata yake huku akibainisha kuwa mke wake ndiye anayeshitakiana na Mchungaji Paulo Lwiva kwa kuwa familia ya mke wake ilikuwa na mgogogoro na familia ya Lwiva kabla ya kuoana lakini anashangaa jina lake kuhusishwa ili kuchafuliwa kisiasa na kuomba jambo hilo limalizwe kisheria kwa kuwa lipo mikononi mwa vyombo vya sheria.