NA JOSEA K. SINKALA.
Mkuu wa Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe Esther Mahawe amewataka watumishi wa Umma Wilayani humo kuendelea kuzingatia uadilifu na kuwa mfano mwema katika jamii zinazowazunguka.
Mkuu Mahawe amewaasa watumishi katika Sekta mbalimbali kutumika vema ili waache alama njema katika maeneo ya kazi wanayohama au kuhamishiwa.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Mbozi Esther A. Mahawe amesema hayo alipokutana na Kamati ya Lishe ya Wilaya hiyo na kuhimiza umuhimu wa lishe bora hususani kwa watoto ili kuepukana na magonjwa yasiyo ya lazima kutokana na kutowapatia lishe bora.
Amesema ni muhimu watoto kulindwa katika jamii dhidi ya matukio mbalimbali ya unyanyasaji ikiwemo ulawiti na ubakaji ili kusaidia kujenga kizazi imara cha sasa na baadaye.
“Katika maeneo yenu ya kazi mhakikishe mnatumia nafasi zenu kuleta mabadiliko chanya kwa kutengeneza hadithi zitakazosomwa vizuri hata mkihamia maeneo mengine”, amesisitiza mkuu wa Wilaya ya Mbozi Songwe, Ester Alexander Mahawe angali akizungumza na Kamati ya Lishe Wilayani humo.