Home KITAIFA DC MAHAWE AZITAKA NGOs KUWASILISHA MIPANGO KAZI YAO

DC MAHAWE AZITAKA NGOs KUWASILISHA MIPANGO KAZI YAO

NA ENEA MWANJA, MBOZI SONGWE.

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi (DC) Mkoani Songwe, Esther Alexander Mahawe ameyaagiza Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) kuwasilisha mipango kazi yao ya kila robo ya mwaka ili kujua mambo yaliyotekelezwa na yanayotarajiwa kutekelezwa na mashirika hayo katika wilaya hiyo.

Mkuu huyo ametoa maagizo hayo Jumanne hii (Juni 13, 2023) katika kikao chake na Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mbozi mkoani Songwe.

Katika kikao hicho mashirika 15 yalishiriki ambayo ni Shaloom, SHIDEFA, Good Neighbour, Cafe Africa, ADP-Mbozi, WISCO, HIMSO, SAWA na Save the Children.

Mashirika mengine yaliyoshiriki kikao hicho ni WAKINA Foundation, HRNS, BLACK Maendeleo, PESCODE, MVITA na Envirocare.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu huyo wa Wilaya ameyataka mashirika hayo kutanguliza uzalendo katika utendaji wao.

“Katika utendaji wenu maudhui yafuate mila na desturi. Uzalendo utangulie ili misaada isijegeuka miba” amesema Mahawe na kuongeza.

“NGO’s zinazofanana zifanye kazi kwa kushirikana ili kuleta ufanisi katika jamii”, amesema Dc Mahawe.

Amesisitiza kuwa kabla ya Asasi au mashirika hayo kupeleka mradi kwa jamii wahakikishe wanataarifu Serikali ya wilaya ili uongozi wa Wilaya kuutambulisha mradi na kuwatambulisha kwa jamii hasa kupitia mikutano ya hadhara.

Ameyataka mashirika hayo kuhamasisha na kutoa elimu ya uzalishaji kwa wanawake na vijana hasa kwa wakulima wa kahawa ili makundi hayo yatambulike ushiriki wao katika kilimo.

Akizungumzia kuhusu mikopo, ameyataka mashirika hayo kuwahamasisha wanaopewa mikopo kuirejesha badala ya kukimbia familia.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbozi, Abbdalah Nandonde, ameyataka mashirika hayo kufanya kazi kulingana na usajili wao.

Amesema kuwa mashirika yanayotoa elimu ya kijinsia yazingatie maadili.

“Lazima tuangalie kinachofundishwa kinaendana na maadili hasa masuala ya kijinsia. Tusije tukajikuta baada ya miezi mitatu wamebadili wanachofundisha. Tuangalie kwenye masuala ya kijinsia kuwa tuko salama isije ikawa baada ya miezi mitatu Mbozi yetu ikaharibika” ametahadharisha Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Mbozi mkoani Songwe.

Previous articleWAZIRI MKUU ATOA MAELEKEZO KWA WIZARA YA MAJI
Next articleMUUGUZI MBARONI KWA KUMBAKA MJAMZITO _ MAGAZETINI LEO JUMATANO JUNI 14/2023

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here