Mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe Claudia Kitta ametoa wito na kuwakaribisha wenye nia ya uwekezaji kuwekeza kwenye vivutio vya utalii ndani ya wilaya hiyo.
Ametoa wito huo wakati wa uzinduzi wa mpango wa uhamasishaji na kutembelea vivutio vya utalii ndani ya wilaya hiyo ulioratibiwa na kikundi cha Sinai Art’s Group ambapo amebainisha kuwa miongoni mwa rasilimali za utalii zilizopo kwenye wilaya hiyo ni pamoja na misitu ya Nyumbanitu,jiwe la ramani ya Afrika,daraja la Mungu na utamaduni wa kuvutia.
“Nitoe wito na kuwakaribisha watu kuja kuwekeza katika maeneo yetu ya vivutio tulivyo navyo tukianzia na Mpanga-Kipengere ambapo tayari serikali imewekeza sana”alisema Claudia Kitta DC wa Wanging’ombe
Danford Mpumilwa ni mstaafu ambaye alikuwa ni mtumishi wa serikali katika sekta ya habari ni mlezi wa kikundi hicho ambapo pia kupitia mpango huo kimezindua filamu ya utalii amesema filamu iliyozinduliwa na kikundi hicho imeonyesha maudhui ya kivutio cha Mpanga Kipengere na kupokelewa vizuri na watu mbali mbali.
“Hii ni hatua kwa kweli licha ya kuwa changamoto kubwa ni uchumi ila niipongeze serikali kwa kuwa na mipango hii ya kukopesha vikundi na sisi tunajipanga huko”amesema Mpumilwa
Meneja wa pori la akiba la Mpanga kipengere Donasian Makoi amesema mpango wa kukuza na kutangaza utalii katika hifadhi hiyo kutokana umuhimu wake mkubwa umekuja kwa kuwa ni msaada mkubwa katika kupeleka maji kwenye mito mitatu mikubwa inayozalisha umeme kwa nchi nzima kauli iliyoungwa mkono na Alphonce Mng’ong’o afisa wanyamapori mkuu.
Kwa Upande wake katibu mkuu kiongozi mstaafu mzee Philimon Luhanjo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika tukio hio, wakati akizindua filamu hiyo ameitaka Wizara ya maliasili na utalii kuona umuhimu wa kuendelea kuvitumia vikundi mbali mbali katika kutangaza utalii Kitaifa na kimataifa.