Na Joel Maduka, Geita
Mkuu wa wilaya ya Chato Mhandisi Deusdedith Katwale amekanusha uvumi unaoendelea katika mitandao ya kijamii kuhusu kutoweka na kupotea kwa wanyama katika hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato iliyoko wilayani humo ambapo amewataka Wanachato pamoja Watanzania kupuuza uvumi huo.
Akizungumza na wandishi wa habari mara baada ya kutembelea hifadhi hiyo na kujionea vivutio vya wanyama na ndege katika hifadhi hiyo ya Taifa katika kuelekea Utalii Chato Festival 2023 inayofanyika wilayani humo Mhandisi Katwale ameshuhudia makundi mbalimbali ya wanyama na ndege katika hifadhi hiyo huku akiwataka watanzania kutembelea hifadhi maalumu yenye upekee.
“Kumekuwepo na upotoshaji mwingi kuhusiana na hifadhi hii kwamba kuna wanyama wameletwa, tumekuja kwa nia na lengo mahususi kuwaonesha watanzania na dunia nzima kwa kwamba hifadhi ya Burigi chato inafanya kazi na ina wanyama mahususi wazuri ambao kwa sehemu kubwa sana hawapatikani sehemu nyingine, ” DC, Katwale.
Kwa upande wake Mhifadhi Mwandamizi Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato Ombeni Hingi amesema hifadhi hiyo ni ya kipekee kwani imezungukwa na maziwa matano likiwemo Ziwa Burigi, Ziwa Ngoma, Ziwa Kasenga na Ziwa Nyamalebe ambapo yamekuwa vivutio vikubwa kwa watalii kufika katika hifadhi hiyo.
Hingi amesema Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato inao wanyama wake wa asili tangu kuanzishwa kwake na hakuna mnyama ambaye aliwahi kuletwa kutoka mbuga nyingine kama ambavyo tumekuwa tukiona katika mijadala mbalimbali ya mitandao ya kijamii.