NA DENIS SINKONDE, SONGWE
MKUU wa wilaya ya ileje mkoani Songwe Mhe Farida Mgomi amewataka wasimamizi wa mradi wa Boost kuwa na uchungu na fedha zilizotolewa na serkali ili zitumike kwa lengo lililokusudiwa.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ikumbilo kata ya Chitete wilayani humo Mei 16 2023 wakati wa uzinduzi wa mradi wa Boost kiwilaya katika zoezi la uchimbaji wa msingi kwenye eneo inapojengwa shule mpya kwenye kijiji hicho.
Mgomi amewataka wasimamizi wa mradi huo ikiwepo kamati ya BOOST wilaya kuweka uwazi kwenye miradi hiyo ambapo serikali imetoa Zaidi ya bilioni moja na nusu.
Mgomi amesema wananchi wanatakiwa kuwa wa kwanza kulinda mradi huo kwa kuripoti kwenye vyombo husika pindi watakapobaini watu wanaojaribu kuiba hata mfuko mmoja wa saruji au Nondo ili wawajibishwe.
“Kazi ya mradi wa BOOST utekelezwe ipasavyo ole wako ubainike unanymelea fedha hizo nawahakikishieni tutaruka wote juu kwa juu ili wote wanaokwamisha miradi iwe mwisho kwa wilaya Ileje,” amesema Mgomi.
Aidha Mgomi amewataka wananchi kwenye maeneo yaliyonufaika na mradi huu washirikiane na washiriki kwa karibu sana ili takwa la serikali ya awamu ya sita litimie kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi na walimu kwenye maeneo hayo.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Ileje Hermani Njeje amesema nguvu ya wananchi inatakiwa ithaminiwe kwenye mradi huo kwani nguvu yao ithaminiwe ili fedha itakayookolewa itumike kuongeza miundombinu mingine kwenye shule hizo.
Diwani wa kata hiyo Osiwelo Kyomo amewasihi wananchi wa kata hiyo kuonyesha ushirikiano pindi wanapohitajika ili kumaliza kwa wakati huku akimsihi Mhandisi wa wilaya kutowachia mafundi mradi mpaka itakapotokea changamoto akidai hali hiyo itapelekea miradi kutokamilika kwa wakati.
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho Frank Ndimbwa na Atanasi Masebo wameishukuru serkali kwa kuwapa mradi huku wakiomba ushirikiano kwa wananchi wa kata hiyo kuhakikisha lengo la serkali la kupunguza msongaamano kwa wanafunzi wa shule mama ya Ikumbilo linatimia.
Ikumbukwe kuwa Wilaya Ileje imepokea fedha Zaidi ya bilioni Moja na nusu kwa ajili ya kujenga miundombinu ya madarasa kwenye shule Nane za Msingi wilayani humo.