Wananchi wa vijiji vya Yuli kata ya Mlale na Itumba kata ya Itumba wilayani Ileje mkoani Songwe wameonywa kujihusisha na uharibifu wa mazingira na kupelekea kukauka Kwa vyanzo vya maji watashughulikiwa Kwa mujibu wa sheria.
Agizo hilo limetolewa na mkuu wa wilaya ya Ileje Mheshimiwa Farida Mgomi wakati akizungumza na wananchi wa kijiji Cha Iyuli kata ya Mlale katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi baada ya mtaalamu kutoka Kwa Wakala ya Usambazaji Maji Usafi na Usafi Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani humo Mhandisi David Gunza kueleza changamoto ya maji kijijini hapo kusababishwa na kupungua chanzo cha maji kulikotokana na uharibifu wa mazingira karibu na chanzo.
Mheshimiwa Mgomi amepiga marufuku wananchi kuingia kwenye hifadhi ya msitu mlima Ileje kujihusisha na shughuli za binadamu na kuharibu uoto wa asili ambako kumepelekea kuhatarisha maisha ya viumbe vinavyoishi humo.
“Hakuna mwananchi anayeruhusiwa kuingia kwenye hifadhi ya mlima Ileje kuingia bila kibali tukikubaini hatutacheka kwani katika ripoti iliyotolewa na mtaalamu kutoka RUWASA inasema vyanzo vya maji hukauka baada ya kukata miti hovyo,” amesema Mheshimiwa Mgomi.
Mheshimiwa Mgomi amewaagiza viongozi wa kata ya Itumba na na Mlale kusimamia sheria za uharibifu wa mazingira kwa kuwakamata wananchi watakaoingia kwenye hifadhi ya mlima Ileje na kuwachukulia hatua kali ili kuwa fundisho kwa wengine.
Akizungumza katika mkutano huo mtaalamu kutoka Wakala wa Usambazaji Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) David Gunza amesema, kijiji hicho kiliingia kwenye ukosefu wa maji baada ya chanzo cha maji kupungua kutokana na shughuli za binadamu kushika kasi.
Mtendaji wa kijiji hiko Lucy Silwimba akiwasilisha kero mbele ya mkuu wa wilaya hiyo amesema, uharibifu wa mazingira kwenye chanzo cha maji umeshika kasi licha ya kuomba msaada ofisi ya kata hiyo kuwasiliana na uongozi wa kata ya Itumba kudhibiti uharibifu huo ambapo mpaka sasa halijafanikiwa.