NA DENIS SINKONDE, ILEJE.
Mkuu wa wilaya ya Ileje mkoani Songwe Mhe. Farida Mgomi amewataka wananchi wa wilaya hiyo kutunza na kulinda miundombinu ya umeme huku akiwataka kuhakikisha wanatumia umeme kwa usalama.
Mhe. Mgomi ametoa rai hiyo wakati mwenyekiti wa bodi ya wakala wa nishati vijijini REA Janet Mbene katika vijiji vya Ibandi kata ya Kalembo na kijiji cha Shinji kata ya Mbebe akizindua mradi wa nishati mzunguko wa pili katika kata hizo.
Mhe. Mgomi amesema kama umeme umefika kwenye vijiji vyao mnatakiwa kubaini fursa zinazoweza kuwaingizia kipato kwenye maisha ya kila siku.
“Tumeona serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi sana itashangazwa tuanfurahia tu kuwaka kwa taa, badala ya kujitengenezea miradi itakayotumia nishati hiyo”, amesema.Mhe. Mgomi.
Mhe.Mgomi amezitaka halmashauri za vijiji kuhakikisha zinatunza miundombinu ya umeme ikiwepo kudhibiti kuchoma moto na kuharibu nguzo ni marufuku.
“Ni marufuku kuona nguzo zinaharibika kwa kuchoma moto ,nikiliona hili linatokea sitakubaliana nalo kwani serikali imetoa fedha nyingi kwa kuwanufaisha wananchi halafu nyinyi mchome miundombinu “, amesema Mhe.Mgomi.
“Rai yangu mtunze na kulinda miundombinu hii na mhakikishe kuwa matumizi ya umeme yanatumika salama hasa kwa vijana wadogo ameendelea kusema Mhe.Mgomi
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Umeme Vijijini, Janet Mbene amesema kuwa, serikali imeweka historia kupeleka umeme vijijini ikiwemo katika vijiji vya Ibandi na Shinji wilayani Ileje ambayo ilikuwa haijapata umeme tangu uhuru.
“Kwa bahati nzuri fedha za kuendesha nishati vijijini zipo, mama yetu (Rais Samia) anahakikisha kuwa hela haikomi kutokana na vyanzo mbalimbali ambavyo vipo serikalini, lengo la kuleta umeme ni kuchochea uchumi” amesema Mbene.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa REA Mhandisi Hassan Saidy amewatahadharisha wananchi kutokufanya shughuli za kijamii chini ya laini kubwa ya kupitisha umeme.
Pia Mhandisi Said amewahakikishia wananchi wa Ileje kuwa serikali imetoa hela za kutosha kuhakikisha miradi hii sasa inafika katika ngazi za vitongoji na wilaya ya Ileje itafikiwa na Vitongoji zaidi ya mia moja (100).
Meneja wa TANESCO Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi Mhandisi Sotco Nombo amewataka wananchi wa kata hiyo kuomba kuunganishiwa umeme ambapo gharama yake ni Sh.27, 000 kwa maeneo hayo ya vijijini pamoja na kununua kifaa cha UMETA ambacho kinarahisisha kuingiza umeme pindi unapokuwa huna gharama za kusuka waya kwenye nyumba zenu.
“Niwambieni ndugu zangu hata kama utashindwa kusuka waaya kwa ajili ya kuweka umeme kwenye nyumba zenu nunueni kifaa kinaitwa UMETA kwa gharama ya shilingi 50,000 ili upate umeme kwa matumizi ya majumbani”, amesema Mhandisi Nombo,”.