Na mwandishi wetu, Sengerema
Kila mradi mmoja wa maendeleo unakuwa na athari katika eneo lingine. Ni kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima akiongea na waandishi wa habari Aprili 23, 2023 mkoani Mwanza alipokuwa akielezea mradi wa ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi litakavyochochea uchumi na ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi ikiwemo sekta ya utalii.

Malima amesema daraja hilo litakapokamilika litatumika kama lango la utalii kwa kurahisisha usafiri wa kuvifikia vivutio vya utalii vya Mkoa wa Mwanza na mikoa jirani na hatimaye kuchangia pato la Taifa.

Kufuatia umuhimu huo, Malima ametoa onyo kwa baadhi ya watu ambao sio waaminifu wanaoiba vifaa vya miradi ya ujenzi.
“Kuna baadhi ya watu wanaona kuwa wanapoiba vifaa vya miradi ni kama wanamuibia mkandarasi kumbe wanamuibia Rais Samia pamoja na sisi Watanzania” alisema Malima na kuongeza
“Tukikuta duka linalouza vifaa vilivyoibwa kwenye miradi ya ujenzi tutalifunga, na mwenye duka huyo hatafanya tena biashara katika Mkoa wa Mwanza labda akatafute leseni mkoa mwingine na lazima atatueleza mnyororo wote”
Aidha, mkuu huyo wa mkoa ameahidi kutoa ushirikiano wa dhati katika nyanja zote kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo kuhakikisha kwamba mradi huo unakamilika kwa wakati.
Mradi wa ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi umeweza kutoa fursa za ajira 1,001 ambapo zaidi ya asilimia 94 ya walioajiriwa ni wazawa
