Na Mwandishi wetu -Njombe
Wakati Serikali ikitangaza kupanda kwa bei ya mafuta hapo Agosti 2 mwaka huu wadau mbalimbali pamoja na wanasiasa wamelalamikia hatua hiyo na kuitaja kwamba ni chanzo cha kupanda kwa gharama za maisha.
Siku za hivi karibuni EWURA ilipandisha bei ya mafuta kutoka bei ya shilingi elfu 2800 na kuwa elfu 3300 kwa lita jambo ambalo limesababisha nauli kuongezeka kwenye vyombo vya moto na hatimaye kuja kuathiri gharama za maisha.
Katika mkutano wa hadhara wa chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA katika kijiji cha Ilembula wilayani Wanging’ombe mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Njombe Rose Mayemba amesema hatua hiyo ya kupanda kwa bei ya mafuta kumetokana na uzembe wa baadhi ya viongozi wa serikali ambapo pia kutasababisha wananchi kuingia kwenye mkwamo wa maisha kwa kuwa gharama za bidhaa nyingi zitapanda zaidi.
Kufuatia CHADEMA kutofurahishwa na mwenendo wa biashara ya mafuta nchini ,wakazi wa mkoa wa Njombe akiwemo Erick Erasto ambaye ni bodaboda wanasema kupanda kwa bei ya mafuta na wakati mwingine kuadimika kumesababisha kupanda kwa gharama za maisha huku wakitaka serikali kuendelea kuweka ruzuku ili kushusha bei.
Wakati mwenyekiti akihoji kupanda kwa gharama za mafuta na athari zake kwa jamii ,Chama hicho kupitia kwa katibu wa mkoa Baraka Kivambe na Rose Mbala mwenyekiti wa Bawacha wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya pia wametaka wananchi kuhoji matumizi ya michango ya maendeleo wanayochangia.