Home KITAIFA CHADEMA SONGWE CHAIBUA UFISADI TUNDUMA, CHAMUOMBA RAIS SAMIA KUFUATILIA

CHADEMA SONGWE CHAIBUA UFISADI TUNDUMA, CHAMUOMBA RAIS SAMIA KUFUATILIA

NA JOSEA SINKALA, TUNDUMA SONGWE.

Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Songwe Isakwisa Lupembe, amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuongeza nguvu kwenye uangalizi wa fedha za umma akisema viongozi wa Wilaya ya Momba na mkoa wa Songwe hawasimamii ipasavyo upotevu wa fedha za Umma.

Lupembe ametoa kauli hiyo kwenye mazungumzo yake na Jambo Media Blog baada ya mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Uwanjani mjini Tunduma.

“Nataka nimwambie Rais Samia Suluhu Hassan huku chini kuna wizi, Soko la Machinga karibia Mill.400 hakuna kitu na hata Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Songwe amekuja hapo naye hajaridhika na matumizi ya fedha hizo na kuna watu wamekamatwa lakini wanakamatwa wa huku chini. Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji Tunduma, Mkuu wa Wilaya (Momba) na Mkuu wa mkoa (Songwe) bado hawasimamii fedha za wananchi, ukienda stendi ya Tunduma pale Mpemba kuna matumizi mabaya ya fedha kwahiyo nimuombe Mhe.Rais atume wataalam waje wachunguze miradi hapa Tunduma”, Ameeleza Isakwisa Lupembe, Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Songwe.

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Tunduma Frank Mwakajoka amesema madiwani walipita bila kupingwa katika uchaguzi mkuu uliopita ndio maana hawana uchungu na maisha ya wananchi ikiwemo kufuatilia miradi na fedha zinazotolewa na Serikali na kuliwa na baadhi ya vigogo serikalini.

Naye Mjumbe wa Kamati tendaji ya CHADEMA Jimbo la Tunduma Herode Jivava, naye ameuangukia Uongozi wa Halmashauri ya Tunduma akiutuhumu kufuja fedha za umma akisema kuna wizi kwenye miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo miradi ya Shule na ujenzi wa Kituo cha mabasi Mpemba.

“Niombe Serikali kuu ije hapa Tunduma ifanye uchunguzi wa kina kwenye miradi yote hapa hata hii shule hapa (S/M Mwaka Uwanjani) pesa zilikuja hakuna kinachofanyika, pale Mpemba ujenzi wa kituo cha Mabasi hela zimepigwa na Polisi mpo, TAKUKURU mpo”, amehoji Herode Jivava, Mjumbe Kamati ya Chadema Jimbo la Tunduma na Mgombea Udiwani Tunduma Mjini (2020).

Katika mkutano huo pia CHADEMA kimesema Katiba mpya ni agenda yao mama kuongoza wananchi katika vuguvugu hilo na ni agenda inayotakiwa kuwa endelevu ili baadaye kupata Tume huru ya uchaguzi katika kuwafanya watanzania kupata viongozi wanaowataka ili kuwatumikia.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Jimbo la Tunduma na Mkoa wa Songwe kinaibua hayo ikiwa ni mkutano wake wa kwanza kufanyika tangu kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara na kufunguliwa rasmi na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho kikuu cha Upinzani (Tanzania Bara) Freeman Aikael Mbowe na Chadema mjini humo kinasisitiza kuendelea na mikutano hiyo ili kueleza itikadi na ilani yake kwa wananchi pamoja na utendaji kazi wa Serikali ambao CHADEMA kinasema sio mzuri.

Previous articleMPISHI AVUNJA REKODI BAADA YA KUPIKA KWA ZAIDI YA SAA 90 BILA KUKOMA
Next articleWANAFUNZI 593 WANUFAIKA NA SAMIA SCHOLARSHIP

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here