Home KITAIFA CHADEMA RUKWA WAKOSOA MKATABA WA BANDARI  

CHADEMA RUKWA WAKOSOA MKATABA WA BANDARI  

 

NA JOSEA SINKALA, RUKWA.

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Sumbawanga mjini kimefanya mkutano wa hadhara katika Kata ya Katandala na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali ambao wameonekana kukosoa mkataba wa bandari kwa madai kuwa una kasoro nyingi na hauna maslahi kwa Taifa (Tanzania).

Akizungumza kwenye mkutano huo mgeni rasmi ambaye ni Katibu wa CHADEMA Kanda ya Nyasa Gwamaka Mbughi amesema Katiba mpya na bora itakuwa majibu ya kiuwajibikaji katika kulinda nchi na raslimali zake badala ya katiba ya sasa iliyopitwa na wakati na haina meno ya kumwajibisha Kiongozi anapokosea.

Gwamaka amesema Mahakama kuu Kanda ya Mbeya ilibaini mapungufu mbalimbali kwenye kesi iliyofunguliwa na walalamikaji kupinga mkataba wa Bandari lakini pamoja na madhaifu hayo haikuwa na uwezo wa kuingilia mhimili wa Bunge kutokana na kuingiliwa na Serikali hivyo kukosa nguvu ambayo ilipaswa iwe nayo.

“Ndugu zangu Chama Cha Mapinduzi kimekuwa kikipotosha, waliokwenda kufungua kesi waliitaka Mahakama iseme ule ni mkataba au makubaliano, Mahakama ikasema ni mkataba kama sisi tunavyosema tofauti na CCM na Serikali yake wanaosema ni makubaliano”, Amesema Gwamaka Mbughi Katibu wa Kanda ya Nyasa Chadema na kuongeza.

“La pili waleta maombi walikwenda kuhoji mahakamani je Dubai ni nchi? Kwa sababu kwa mujibu wa sheria za kimataifa mkataba unapaswa kuwa baina ya nchi na nchi na sio baina ya nchi na mkoa, kwahiyo walioenda mahakamani walienda kuhoji kwanini Tanzania iliingia mkataba na Dubai ambayo kwa mujibu wa sheria za kimataifa sio nchi na wananchi wa Rukwa mnapaswa kufahamu Dubai nikama ilivyo Zanzibar, ni sehemu ya Tanzania hivyohivyo Dubai ni sehemu ya Falme za kiarabu”, Amesisitiza Katibu Gwamaka.

Hata hivyo amewataka wananchi mkoani Rukwa, Kanda ya Nyasa na nchini kwa ujumla kukiunga mkono Chama hicho (CHADEMA) kwa kujisajili kwenye mfumo wa kidigitali na kuzidi kujiimarisha ili kwenda kufanya uchaguzi wa haki mwakani (uchaguzi wa serikali za mitaa 2024) na mwaka 2025 kwenye uchaguzi mkuu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Rukwa Sadrick Malila (Ikuwo), amewataka wananchi kuungana na viongozi na wanachama wa Chama hicho kukataa kusainiwa kwa mkataba wa bandari kati ya Tanzania na Kampuni ya DP World ya falme za Uarabu kwakuwa mkataba huo ni tata, unavunja hadhi ya nchi na kutoa nafasi kubwa ya kiuchumi kwa wageni badala ya kumfaidisha M-Tanzania.

Ikuwo amesema Serikali imeshindwa kuwaletea maendeleo wananchi wake hivyo kudai kuwa mabadiliko lazima yaanze na wana Sumbawanga wenyewe kwa kuchagua viongozi bora kuanzia kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa.

“Ndugu zangu mkataba wenyewe ni ajali, wewe una nyumba, unataka kumpangisha mpangaji anayeandika mkataba si ni mwenye nyumba sasa sisi bandari zote ni za kwetu lakini wametuandikia mkataba je sisi ni mambumbumbu! Uwekezaji ni sawa lakini kwa Mkataba huu hapana”, Sadrick Malila.

Naye Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini Aida Kenani amesema yeye ni mmoja kati ya wabunge waliokwenda Dubai akidhani ni kwa ajili ya kujifunza namna Dubai inavyoendesha Bandari lakini matokeo yake ikawa tofauti kwa kuingia mkataba usiokuwa na maslahi kwa nchi hivyo kugomewa na wananchi.

“Haihitaji Malaika Gabrieli kuja kubadilisha maisha yetu ila inahitaji mfumo ambao viongozi wanatokana na maamuzi ya wananchi, leo kuanzia wenyeviti wa vijiji ni viti maalum. Unaposema mtu alipita bila kupingwa huyo ni special seat (Viti maalum), ukienda kwa madiwani nao walipewa sadaka hadi huko juu (Taifa). Leo maovu yaliyofika hadi Bungeni yanatokana na mfumo mbaya kwasababu hakuna mfumo uliowekwa na wananchi, hawawezi kukaa na wananchi kujadili mambo yanayowahusu wananchi”, Aida Kenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini.

“Mimi ni miongozi mwa wabunge waliokwenda Dubai, kwenye mkoa wa Mkoa wa Rukwa mimi ni Mbunge pekee niliyekwenda Dubai, kwahiyo ukisikia wengine wanasema waambie kaa kimya azungumze aliyekwenda Dubai”, amesimulia Mbunge Aida.

Hatahivyo Mbunge Aida Kenani mbunge pekee wa CHADEMA amesema hakuna anayepinga uwekezaji katika kuchochea maendeleo ya nchi lakini tatizo ni ubovu wa mkataba ambao si shirikishi na faida kwa wananchi.

“Ndugu zangu ni kweli kwamba nilikwenda Dubai Januari 28-Februali 02, 2023) na nilipokuwa nakwenda sikujua jambo lolote lililoko nyuma ya pazia, nilijua tunakwenda kama Bunge tujifunze wenzetu wanafaulu vipi kuendesha Bandari na sisi Tanzania tumefeli wapi kuendesha Bandari lakini ukiziangalia hizo tarehe nikama maigizo, sisi Bunge tunakwenda wakati mkataba ulishasainiwa, miongoni mwa wabunge waliopiga kura ya hapana bungeni ni mimi hapa kwenye jambo hilo na ndio maana CHADEMA tulisema tunataka tutofautishe kati ya wateule na wawakilishi wa wananchi, mwakilishi wa wananchi anawasikiliza wananchi juu ya mawazo yao ndio anaenda kufanya maamuzi juu ya yale aliyoambiwa”, Aida Kenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini.

Mbunge Aida amesema Bunge la Tanzania limekuwa la maigizo badala ya kuishi uhalisia wa kujadili kero za wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali badala yake limekuwa likipokea maelekezo ya Serikali bila kushauri.

Previous articleDC JOKATE AAHIDI KUWA BALOZI WA ZAO LA MKONGE
Next articleMAADHIMISHO YA MIAKA 62 YA UHURU KUFANYIKA KILELE CHA MLIMA KILIMANJARO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here