Wafanyabiashara wa Tanzania katika Halmashauri ya Mji Tunduma Wilaya ya Momba mkoani Songwe wako hatarini kupoteza mitaji yao na kukwamishwa uchumi wa Taifa kufuatia biashara yao ya zao la mahindi kuzuiwa nchini Zambia tangu walipoyanunua kwa Serikali ya Zambia mwishoni mwa mwaka jana (2022).
Kwa mujibu wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Tunduma Mkoani Songwe Frank Mwakajoka hali hiyo imedumu kwa muda sasa lakini bado wafanyabiashara wa Tunduma wanazungushwa hivyo kukwamishwa kiuchumi na uchumi wa nchi hasa eneo hilo ambalo ni lango kuu la kiuchumi katika nchi zilizoko Kusini mwa jangwa la Sahara SADC.
Mwakajoka ameitaka Serikali ya Tanzania kuingilia na kuongeza nguvu juu ya kitendo cha wafanyabiashara wake kuzuiwa biashara yao ya Mahindi walioyanunua nchini Zambia tangu mwishoni mwa mwaka jana hali inayohatarisha kudorola kwa uchumi wa wafanyabiashara hao hasa Halmashauri ya Tunduma Momba mkoani Songwe.
Mwakajoka amesema hayo wakati akizungumza na mamia ya wanachama wa CHADEMA na wananchi waliojitokeza kusikiliza mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Mwaka Kata ya Uwanjani mjini Tunduma.
Mbunge huyo wa zamani wa Jimbo lake la Tunduma (2015-2020) amesema wafanyabiashara wa Tanzania walianza kununua mahindi Juni 2022 nchini Zambia na kuyauza katika eneo maarufu la biashara la Nakonde lakini cha ajabu ilipofika Novemba 2022 Serikali ya Zambia ilianza kugoma kuwapatia mahindi walio lipia wafanyabiashara hao wa Tanzania.
Amesema baadaye walilalamika kwa Balozi wa Tanzania nchini Zambia ndipo wachache wakapewa lakini hata waliopewa baada ya kupakia mahindi hayo yamezuwiliwa njiani ikiwemo katika maeneo ya Kapilimposhi na Kasama kabla ya kuyashusha sokoni Nakonde.
“Wafanyabiashara walionunua mahindi Zambia yamezuiliwa Nakonde, Kapilimposhi, Mpika, Kasama, Lusaka na maeneo mbalimbali nchini Zambia na Mahindi waliuziwa na NFRA ya Zambia baadhi wamewapa permit (kibali) na mengine bado hawajatoa permit hata yenye permit yaliyopakiliwa huko Lusaka na maeneo mengine yamezuiliwa hapo Nakonde”, amesema Mwakajoka na kuongeza.
“Mahindi hayo yalinunuliwa huko ili yauzwe hapa Nakonde Zambia na siyo kuyavusha kuja Tanzania, kinachoshangaza nikwamba Serikali ya Zambia imeuza mahindi alafu inazuia yasifike Sokoni hapa Nakonde, na kama Serikali ya Zambia inayataka Mahindi basi iwarudishie pesa wafanyabiashara hao ambao ni wengi mno”, ameeleza Mbunge huyo wa Zamani ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya wagombea wa CHADEMA Kanda ya Nyasa (Nyanda za juu kusini).
Pamoja na hayo amemshukuru Balozi huyo kwa juhudi alizofanya kuhakikisha baadhi ya mahindi wanapewa wafanyabiashara hao licha ya Zambia kwenda kuyazuia sokoni Nakonde ili kuepusha hasara inayoweza kutokea kwa wafanyabiashara hivyo kumwomba Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufuatilia suala hilo.
“Tunamuomba Mhe. Rais aingilie kati suala la wafanyabiashara hawa ambao wanataka kudhurumiwa mahindi waliyoyanunua kihalali baada ya Serikali ya Zambia kuanza kuuza mahindi yake kwenye hifadhi yao ya Chakula (Taifa lao), sasa kosa letu liko wapi mpaka tuanze kubaishwa na kutaka kutunyang’anya Mahindi tuliyonunua kihalali hivyo nakuomba Mhe. Rais kwa mamlaka uliyo nayo kama Kiongozi wetu tunaomba uingilie kati ili kuokoa mitaji ya wa Tanzania hawa”, Amesisitiza Frank Mwakajoka.
Wakati huohuo Mwakajoka alitumia hadhara hiyo kuitaka Serikali ya mkoa kupitia Mkuu wa mkoa wa Songwe Dkt. Francis Michael kutuma timu ya wataalam wa kwenda kufanya uchunguzi wa fedha za umma anazodai zimeliwa katika miradi mbalimbali mjini Tunduma ikiwemo kwenye kituo cha mabasi Mpemba Tunduma kilichotengewa fedha zaidi ya Bil. 1.5 lakini ujenzi wake haueleweki.