Na Josea Sinkala, Mbeya.
Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mbeya Vijijini (Kichama) kimekataa kukagua miradi mitatu ya Maji katika kata za Ijombe, Itewe na Inyala baada ya kutoridhika na taarifa ya utekelezwaji mradi wa maji Tembela – Iyawaya uliyokuwa umeandaliwa bila kuwepo thamani halisi ya mradi huo (BOQ) hatua inayokwamisha dhamira ya Serikali kutatua kero ya maji.
Miradi iliyokataliwa kukaguliwa ni mradi wa Maji Tembela Iyawaya, Mradi wa Maji Galijembe na Mradi wa Maji Nsongwi Mantanji.
Hayo yamejiri baada ya Kaimu Meneja wa Wakala wa maji vijijini Ruwasa Wilayani humo Mhandisi Mwachembe Mjeni kumaliza kutoa taarifa ya mradi wa maji Iyawaya Tembela unaotarajiwa kuwa mkombozi kwa wananchi zaidi ya Elfu nne wa kata ya Itewe na kijiji kimoja cha kata ya Inyala.
Wakizungumza kwenye mradi huo, wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mbeya vijijini (Kichama) wameipongeza Serikali kwa kudhamiria kutatua kero ya maji kwa wananchi lakinu wakaeleza mapungufu mbalimbali ya mradi huo wa maji ikiwemo kwenda kwa kusuasua hivyo kuonyesha mashaka ya kutokamilika kwa wakati.
Katibu wa CCM Wilaya ya Mbeya Vijijini Rehema Nzunye ameeleza kukerwa na tabia ya Chama kutoa maelekezo ya mara kwa mara kwa watendaji lakini utekelezaji umekuwa wa kusuasua.
Akihitimisha ziara hiyo Mwenyekiti wa CCM Mbeya vijijini Akimu Sebastian Mwalupindi amesitisha ziara hiyo iliyokuwa ifuate mradi wa Maji Nsongwi juu – Nsongwi Mantanji na Galijembe baada ya thamani ya mradi kutoonekana kwenye taarifa hiyo ambayo pia haijabainisha inaenda kwa nani baada ya Ruwasa kueleza kwamba taarifa zote ziko kwa mfumo mmoja.
Mradi wa Maji Iyawaya Tembela unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2023 na kunufaisha wananchi zaidi ya elfu nne wa vijiji vya Isongwa, Tembela, Iyela nyala, Idunda kata ya Itewe na kijiji cha Iyawaya Kata ya Inyala Wilayani Mbeya hivyo Wizara ya maji kupitia wataalam wake wanapashwa kwa kadri ya utolewaji wa fedha kuhakikisha wanatekeleza miradi ya maji kwa kiwango na kwa wakati ili kuwasaidia wananchi lengwa kama ambavyo imedhamiriwa kumtua mama ndoo kichwani na Ruwasa wakiendelea na kaulimbiu yao ya Maji Bombani.