Home KITAIFA BWAWA LA JULIUS NYERERE LADHIBITI MAFURIKO  

BWAWA LA JULIUS NYERERE LADHIBITI MAFURIKO  

Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba akikagua maendeleo ya ujenzi wa tuta kuu la kuzui maji ili kutengeneza bwawa

Waziri wa Nishati Mhe.January Makamba akikagua maendeleo ya ujazaji wa maji katika bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere kwa kutumia boti maalamu

 

Na Agnes Njaala, Rufiji

Mradi wa kufua Umeme wa Julius Nyerere umeanza kuonyesha faida baada ya kuzuia mafuriko katika baadhi ya mikoa ya Pwani na Morogoro.

Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba akiwa katika ziara ya kujionea ujazaji katika Bwawa leo Jumanne ,25 Aprili 2023 amewaambia waandishi wa habari kuwa zoezi la ujazaji maji kwa kiasi kikubwa imezuia mafuriko yaliyokuwa yakiathiri wananchi.

“Tunafurahi kwamba tayari tumefikia mojawapo ya malengo makubwa ya kuanzishwa kwa mradi huu ambayo ilikuwa ni kuwakinga wananchi dhidi ya madhara yatokanayo na mafuriko” alisema Mhe.Makamba.

Waziri Makamba ameleza kuwa kiasi cha mvua kilichoingia kwenye bwawa mwezi huu kinafanana na kile kilichonyesha miaka mitatu iliyopita na kuleta mafuriko katika mikoa ya Morogoro na Pwani.

“Kwa mvua hizi zilizonyesha katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, na hasa siku mbili zilizopita, leo tungesikia taarifa za vifo na uharibifu wa mali, lakini kutokana na mradi huu, jambo hilo halijatokea mwaka huu,” alisema Waziri Makamba.


Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba akikagua maendeleo ya ujenzi wa tuta kuu la kuzui maji ili kutengeneza bwawa

Akizungumza kuhusu mradi huo kwa ujumla, Waziri Makamba alisema kwa sasa mradi umetekelezwa kwa takribani asilimia 86 na kwamba kiwango cha maji kilichopo kinawapa matumaini juu ya lengo la mradi kuanza uzalishaji ifikapo mwezi Juni, mwaka 2024.

Waziri wa Nishati Mhe.January Makamba akizungumza na waandishi wa habari juu ya maendeleo ya ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere ambao umefikia asilimia 86

Akifafanua zaidi, Waziri Makamba alisema ili bwawa hilo lianze kuzalisha umeme kwa kiwango chake, linatakiwa kuwa na ujazo wa mita za ujazo bilioni 30 na sasa tayari kuna mita za ujazo bilioni 6 sawa na asilimia 20 ya kiasi kinachotakiwa.

Aidha, Waziri Makamba amewashukuru wataalamu na wafanyakazi wengine kwenye mradi huo kwa kufanya kazi kwa uzalendo na weledi na kuwataka wahakikishe wanamaliza kazi hiyo katika muda uliopangwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Maharage Chande, alimwahidi Waziri kwamba watahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili kupunguza kero ya ukosefu wa umeme hapa nchini.

“Wito wangu kwa wafanyakazi wenzangu wa TANESCO ni kwamba tusianze kuzembea kwa sababu tunaona kazi inakaribia kumalizika, huu ndio wakati wa kuchapa kazi bila kuchoka,” alisema Chande.

Mwezi Disemba 22 mwaka jana (2022), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi zoezi la kuanza kujaza maji katika mradi huo unaotarajiwa kuzalisha Megawati 2115 mara utakapokamilika.

Previous article‘MAJI BWAWA LA NYERERE YAFIKIA MITA ZA UJAZO BILIONI 6’ – WAZIRI MAKAMBA
Next articleWIMBI LA TALAKA KWA WANANDOA LAZIDI KUTIKISA… BALEKE MAYELE WAMOTO KIMATAIFA _MAGAZETINI LEO JUMATANO APRILI 26/2023

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here