Home KIMATAIFA BENKI YA DUNIA YAENDELEA KUWEKEZA KWENYE MAENDELEO YA SEKTA BINAFSI

BENKI YA DUNIA YAENDELEA KUWEKEZA KWENYE MAENDELEO YA SEKTA BINAFSI

 

 

Na Benny Mwaipaja, Washington DC

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameishukuru Taasisi ya Benki ya Dunia inayotoa mikopo na misaada kwa sekta binafsi (Internationa Finance Corporation-IFC), kwa kuwekeza zaidi ya dola za Marekani milioni 370 kwa ajili ya kuendeleza sekta hiyo nchini.

 

Dkt. Nchemba amesma hayo alipoongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano na Makamu wa Rais wa Taasisi hiyo, Bw. Sergio Pimenta, kando ya mikutano ya Kipupewe iliyoandaliwa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la KImataifa (IMF), Jijini Washington D.C, nchini Marekani.

 

Dkt. Nchemba alisema kuwa mchango wa Taasisi hiyo katika kuisaidia sekta binafsi ni muhimu kwa kuwa itasaidia kukuza ajira kwa vijana, mitaji, teknolojia na kuweka mazingira ya uchumi jumuishi katika jamii.

 

“Ninaishukuru taasisi yako kwa kuchangia maendeleo ya sekta binafsi nchini Tanzania katika nyanja za sekta ya fedha, uzalishaji viwandani, huduma na nishati, tunaamini hatua hiyo itaendelezwa zaidi ili tuweze kupiga vita umasikini na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kukuza uchumi wa nchi” alisema Dkt. Nchemba

 

Aliiomba Taasisi hiyo kuongeza kiwango cha fedha kwa ajili ya kusaidia ukuaji wa kasi wa sekta binafsi nchini Tanzania kutokana umuhimu wake katika kukuza uchumi na maendeleo ya nchi, kutoka kiwango cha sasa cha dola milioni 372 hadi kufikia zaidi ya dola za Marekani milioni 700.

 

Dkt. Nchemba alisema kuwa sekta binafsi ni injini ya ukuaji uchumi hivyo uwekezaji mkubwa wa rasilimali fedha unahitajika ili sekta hiyo iweze kuchochea shughuli za uzalishaji na maendeleo ikiwemo kilimo na mifugo, nishati, na maeneo mengine mtambuka ili kuleta tija katika sekta hizo na hatimaye kuchangia katika pato la Taifa.

 

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, alimwamweleza Kioongozi huyo kuwa Zanzibar inahitaji kuwa na sekta binafsi imara kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya nchi.

 

Alisema kuwa Serikali inatekeleza Sera ya Uchumi wa Buluu ambayo inahitaji nguvu ya Sekta Binafsi akitolea mfano wa mpango wa Serikali wa kujenga Bandari kubwa ya Somanga fungu, ambayo inahitaji ushiriki wa Sekta binafsi.

 

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia wa Taasisi inayotoa mikopo na misaada kwa Sekta binafsi, Bw. Sergio Pimenta, aliahidi kwamba Taasisi yake inatarajia kuongeza kiwango cha uwekezaji wa mitaji kwa sekta binafsi nchini Tanzania hivi karibuni.

 

Alisema kuwa Tanzania inaendelea kufanya vizuri katika kuvutia uwekezaji ambapo taasisi na kampuni kadhaa zimeonesha nia ya kuwekeza nchini humo, baada ya mkutano wa uwekezaji uliohusisha wadau kutoka kila pembe ya dunia waliokutana Jijini Dar es Salaam mwaka jana, 2022.

 

“Kutokana na umuhimu wa Tanzania katika kufanya mageuzi yake ya kiuchumi, tunatarajia kufanya kazi kubwa ya kuwashawishi wadau wetu kuwekeza mitaji na teknolojia nchini Tanzania na kutokana na umuhimu huohuo, tunatarajia kufungua ofisi ya kudumu itakayokuwa ikitumika kuratibu masuala ya kuvutia uwekezaji” Alisema Bw. Pimenta

 

Mafanikio haya ni matokeo ya mkutano kati ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mkurugenzi Mtendaji wa IFC, Bw. Makhtar Diop, wakati wa ziara yake aliyoifanya nchini Tanzania mwezi Februari 2022, ambapo alimwomba Kiongozi huyo kuisadia sekta binafsi ili iweze kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa

 

Utekelezaji wa mipango hiyo ya kuiwezesha sekta binafsi utasaidia kutekeleza Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wenye thamani za shilingi trilion 114.8 ambao umeainisha kuwa asilimia 40 ya utekelezaji wa mpango huo sawa na shilingi trilioni 40.6 zinatakiwa kutoka katika sekta binafsi huku asilimia 60 ya gharama za mpango huo sawa na shilingi trilioni 74.2 zinatakiwa kutoka Serikalini.

Previous articleUCHUMI WAPAA ◾ PATO LA TAIFA LAFIKIA SH TRIL 200…..AVUNJA KITUO CHA POLISI,AINGIA NA KUJISAIDIA _ MAGAZETINI LEO JUMAPILI APRILI 16/2023
Next articleSHIRIKISHO LA VYAMA VYA WAFANYAKAZI TANZANIA, LAONYESHA UBAGUZI MEI MOSI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here