Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro limepokea taarifa ya kamati ndogo iliyoundwa kwaajili ya kufuatilia uharibifu wa mazingira katika wilaya hiyo huku kamati hiyo ikibainisha kuwa upo uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwemo upikaji wa pombe haramu ya gongo katika Halmashauri ya Hai,Moshi Vijijini na Moshi Manispaa katika mto Kilareda,ukataji wa miti pamoja na shughuli za kilimo ndani ya mita sitini.
Akiwasilisha ripoti hiyo Mei 10.2023 Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Diwani Kata ya Mnadani Nasib Mndeme amesema kuwa shughuli hizo za kibinadamu zinahatarisha maisha ya viumbe hai pamoja na kuchoche ukame.
“Wakati wa ukaguzi kamati ya ulinzi na usalama walifanikiwa kukamata mapipa 22 ya pombe ya Gongo, huku wakishuhudia mboga aina ya saladi zikipigwa sumu kali ndani ya maji
“Katika mto huo pande zote zimeharibiwa kwa kukatwa miti,mboga aina ya saladi kuoteshwa ndani ya chemichemi na kupuliziwa sumu kali na shughuli ya upikaji wa pombe haramu ambapo maji taka ya pombe hiyo yanamwagwa ndani ya maji na kuua viumbe hai” alieleza .
Kamati hiyo imeshauri kuwa Halmashauri zote tatu Wilaya ya Hai,Moshi Vijijini na Moshi Manispaa kupanda miti katika maeneo yaliyo haribiwa huku Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Moshi (MUWSA) kuhakikisha wanang’oa mboga zote zilizopandwa ndani ya mito na chemichemi za maji .
Awali akipokea taarifa hiyo Mwenyekiti Halmashauri ya Wilaya ya Hai Edmund Rutaraka amepongeza kazi ilitofanywa na kamati hiyo ndogo huku akimtaka Mkurugenzi kuweka mkakati mzuri wa kuhakikisha mazingira ya Halmashauri hiyo yanatunzwa hasa kwa kupandwa miti kipindi hiki cha mvua