NA JOSEA SINKALA, MBEYA
Mwandishi Habari Mwandamizi mkoani Mbeya Gordon Nisakumbona Kalulunga, amefika Ofisini kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya (RCO) kwa ajili ya mahojiano juu ya Television yake ya mtandaoni (Nyikani Tv) ikiwa imesajiliwa.
Wito wa Kalulunga Polisi unaelezwa kutokana na kuchapishwa Maudhui ya Wakili wa kujitegemea Boniface Mwabukusi mmoja katika jopo la mawakili wanne wanaosimama mahakamani kuwatetea wananchi wanaopinga mkataba wa bnandari alipokuwa akizungumzia kuhusu kupinga mkataba huo wa bandari na kuendesha kesi ambayo kwa sasa inangojewa hukumu juma lijalo.
Video ya wakili huyo ilisambaa siku kadhaa zilizopita kupitia chombo hicho cha habari kabla ya shauri la kupinga mkataba huo kuanza kusikilizwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya.
Kalulunga ameitwa na kuhojiwa baada ya kuitwa mara kadhaa tangu mwezi uliopita akiwa nje ya mkoa kwa masuala ya kikazi ambapo amehojiwa kwa muda wa dakika 51 kisha kuruhusiwa kuondoka akiwa na baadhi ya watu wakiwemo ndugu na Wakili wake Philip Mwakilima.
Hata hivyo mwanahabari huyo amelishukuru Jeshi la Polisi kupitia RCO na wasaidizi wake kwa namna walivyompokea na kumpa ushirikiano juu ya walichokuwa wakitaka kutoka kwake.