Home KITAIFA BANDARI YA DAR ES SALAAM YAWEKA REKODI MPYA KATIKA KUHUDUMIA SHEHENA

BANDARI YA DAR ES SALAAM YAWEKA REKODI MPYA KATIKA KUHUDUMIA SHEHENA

 

Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari ofisini kwake leo Mei 29, 2023

*Hadi kufikia Mei, 2023 yahudumia zaidi ya tani milioni 18*

*Muda wa kuhudumia shehena wapungua hadi kufikia chini ya siku nne*

Na Mwandishi wetu Dar es Salaam

Hadi kufikia Mei, mwaka huu Bandari ya Dar es Salaam imeweza kuhudumia shehena ya mzigo mbalimbali zaidi ya tani milioni 18 kutoka kwenye lengo lililowekwa la kuhudumia tani milioni 19.6 za shehena.

Kwa muda uliobaki, uko uwezekano mkubwa wa kuvuka lengo hadi kufikia kuhudumia tani milioni 20 za shehena jambo ambalo halijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa bandari hiyo.

Hayo yamesemwa leo Mei 29, 2023 na Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Mrisho Mrisho akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu maboresho yaliyofanywa pamoja na utendaji kazi wa bandari hiyo.

Mrisho amesema, bandari hiyo imepita katika michakato mbalimbali ya maboresho kwa lengo la kuongeza ufanisi ikiwemo kuhudumia shehena kwa siku chache zaidi na kutatua changamoto zilizokuwepo.

Ameongeza kuwa, kufuatia maboresho makubwa yaliyofanyika katika bandari hiyo ikiwemo ujenzi wa gati mpya tatu (03), kuongeza kina cha maji kutoka mita 6-7 hadi mita 14.5 na kuboresha magati yaliyokuwepo awali, hali ambayo pamoja na mambo mengine imepunguza muda wa kuhudumia shehena ambapo kwa sasa muda wa kuhudumia shehena hauzidi siku nne.

“Baada ya maboresho katika bandari ya Dar es Salaam Kina cha maji kimeongezeka kutoka mita 6-7 hadi kufikia mita 14.5 na kuwezesha meli kuhudumiwa katika gati lolote ndani ya bandari na bandari ya Dar es Salaam, hatua hii imefanya kuwa na idadi kubwa ya meli zinazohudumiwa katika bandari hii” alisema Mrisho

Kufuatia maboresho hayo, Mrisho ameeleza kuwa, moja ya matokeo chanya yaliyoonekana ni pamoja kuongezeka kwa idadi kubwa ya meli kubwa (Deep sea vessel) zaidi ya 90 kuhudumiwa ndani ya mwezi mmoja.

“Watumiaji wa bandari ya Dar es Salaam wameongezeka sana, hivi sasa kwa mwaka mmoja tu tunahudumia magari kati ya 250,000 hadi 300,000, na 60% ya magari hayo ni ya nchi jirani” alisisitiza Mrisho

Ameendelea kwa kusema kuwa, kwa sasa katika bandari hiyo kuna gati jipya maalum kwa ajili ya kuhudumia shehena ya magari jambo ambalo limeifanya bandari hiyo kuweka rekodi ya kihistoria kwani hapo awali shehena ya magari ililkwa ikihudumiwa kwa kuchanganywa na shehena nyingine.

Akiongelea dhana ya ushiriki wa sekta binafsi na mchango wake katika shughuli za bandari hususan bandari ya Dar es Salaam, Mkurugenzi Mrisho amesema

“Hakuna namna, na ni lazima kuwe na ushiriki wa sekta binafsi katika uendeshaji wa Bandari, na hii inafanyika duniani kote. Kuna vifaa vya uendeshaji wa bandari ni gharama kubwa na fedha zinatoka serikalini, na wakati huo huo serikali inafanya kazi nyingi ikiwemo ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo madarasa, barabara, miradi ya umeme, maji na vyote hivi hutumia fedha”

Matukio mbalimbali katika picha yakimuonesha Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho akielezea utendaji kazi wa sehemu mbalimbali za bandari hiyo

Kwa upande wake mdau wa bandari ambaye pia ni Mkurugenzi wa kampuni ya Uwakala ya Epic Mhandisi Tonny Swai, ametoa wito kwa watumiaji wa bandari kutumia bandari za Tanzania kwa kuwa ni salama, unafuu katika gharama na kutumia muda mchache wa kuhudumia shehena.

Mhandisi Swai amesisitiza kuwa, usalama katika bandari ya Dar es Salaam ni wa kiwango cha juu kwa kuwa kamera za usalama zimefungwa kila kona na hivyo hakuna uwezekano hata kidogo wa wizi wowote kufanyika katika bandari hiyo.

Mdau wa Bandari ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwakala ya Epic, Mhandisi Tonny Swai akiwaelezea waandishi wa habari hali ya utendaji kazi wa bandari ya Dar es Salaam baada ya maboresho makubwa yaliyofanyika katika bandari hiyo

Bandari ya Dar es Salaam ni lango la kuu la kibiashara, asilimia 95 ya biashara ya kimataifa ya Tanzania inahudumiwa na bandari hii. Aidha, bandari hii inahudumia nchi jirani zisizo na bandari kama vile Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Rwanda, Malawi, Uganda na Zimbabwe.

Bandari ya Dar es salaam ni kiungo kikuu cha kibiashara si tu kutoka na kwenda nchi za Afrika Mashariki na kati, bali pia na nchi za Mashariki ya kati, Mashariki ya mbali, Ulaya, Australia na Marekani.

Mwonekano wa baadhi ya maboresho yaliyofanywa katika bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utoaji huduma

Previous articleSERIKALI YAAHIDI KUTAFUTA FEDHA KUJENGA STENDI KAMSAMBA, IKANA MOMBA.
Next articleDKT. GWAJIMA AONGOZA MENEJIMENTI YA WIZARA KUMUAGA MUWAKILISHI MKAZI WA UNICEF

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here