Njombe
Mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa ameisitisha kampuni ya Alliance in Motion Global inayojishughulisha na uuzaji wa bidhaa za tiba lishe kufanya kazi katika wilaya ya Njombe kutokana na kampuni hiyo kutokuwa na usajili wa Brela,kuwa na uthibitisho mfu wa TBS,kutokuwa na TIN Number,kukosa leseni ya biashara pamoja na kukosa utambulisho wa kamati ya ulinzi na usalama.
DC Kissa ametoa maelekezo hayo mara baada ya kupokea taarifa ya kamati ya ulinzi na usalama ambapo pia amebainisha kuwa kampuni hiyo imekuwa ikiwapigia simu watu kutoka mikoa mbali mbali kuja wilayani Njombe kwa ahadi ya kupata kazi jambo ambalo limekuwa likiwaumiza vijana wengi kukaa muda mrefu bila kupata kazi baada ya kufika Njombe.
“Akija huku kwa mategemo ya kupata ajira anaambiwa atoe 30,000/= mara toa 600,000/= sasa nataka niwaambie Njombe sio shamba la bibi wamekwishatengeneza kelele nyingi na nimepokea watu ofisini kwangu kama mara tatu na kutoa nauli ya watu kurudi Dar es Salaam,kwa hiyo hii kampuni ninaisimamisha kufanya kazi hapa Njombe na irudishe nauli za watu kurudi kwao”ameagiza DC Kissa
Ameitaka kampuni hiyo kufanya kazi kwa kufuata taratibu zote ili kuepusha migogoro inayojitokeza kwa kuwa pia kundi la watu linalodanganywa linaweza kuanza kufanya uhalifu baada ya kukutana na mazingira magumu ugenini.