Mfanyabiashara Harid Njianguru,mkazi wa Kidatu Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro anasakwa na polisi kwa tuhuma za kumshambulia mteja wake na kusababishia madhara makubwa baada ya kushindwa kulipa kiingilio cha Sh 500 kuangalia mpira kati ya timu ya soka ya Azam FC na Tanzania Prisons kwenye ukumbi wa baa anayomiliki.
Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro Alex Mkama,amesema tukio hilo lilitokea usiku wa Agosti 28, 2023 katika kijiji cha Mkamba Wilaya ya Kilombero baada ya mfanyabiashara huyo kumshambulia Protas Komba (40) kwa kumpiga na kisha kumsukuma na kuangukia kisogo na kupoteza fahamu.
Amesema Komba alifika baa ya mfanyabiashara huyo ambayo inajulikana kwa jina la Kigamboni’ ili kuangalia mchezo huo na kwamba alishindwa kulipa kiingilio cha sh 500 na akawa analazimisha kuingia ndani ya baa.