Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi imemuachia huru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya Reuben Mfune na mwenzake waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi.
Uamuzi huo umetolewa Agosti 03, 2023 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Ruangwa Mariamu Mchomba baada ya Mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP) kuielezea Mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Inadaiwa kuwa Reuben Mfune na mwenzake walikuwa wakikabiliwa na kosa la uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya shilingi Milioni 51 ambapo Katika kipindi hicho Mfune alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa kuanzia 2012 – 2015
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) ameifuta kesi hiyo chini ya kifungu 91(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 kama ilivyorekebishwa mwaka 2022 ambayo iliwasilishwa na wakili wa Serikali mwandamizi Mwanaamina Kombakono.