Home KITAIFA AKAMATWA KWA TUHUMA YA KUZALISHA NA KUSAMBAZA DAWA BANDIA

AKAMATWA KWA TUHUMA YA KUZALISHA NA KUSAMBAZA DAWA BANDIA

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi limefanikiwa kumkamata Bw. William Japheti Mwangile (39) Mkazi wa Kata ya Kipawa, Halmashauri ya Manispaa la Ilala kwa tuhuma ya kuzalisha na kusambaza dawa bandia kwa mfumo wa makopo kinyume cha kifungu 76 cha Sheria ya dawa na vifaa tiba sura 219.

 

Mkaguzi wa Dawa kutoka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Mashariki, Jafari Mtoro, amesema kuwa mtuhumiwa huyo amekamatwa tarehe 14/4/2023 nyumbani kwake maeneo Kipawa na baada ya kufanyiwa upekuzi katika nyumba yake, wamekamata aina mbalimbali za nebo za dawa 537 zikiwa tayari zimeandikwa majina.

 

Bw. Mtoro amesema pia wamekamata viroba vitatu vya unga, kimoja kikiwa na rangi ya njano, viwili vikiwa na rangi nyeupe ambazo vinazaniwa ni malighafi za dawa.

“Leo tarehe 15/4/2023 usiku wa manane tumekwenda nyumbani kwa wazazi wake kwa ajili ya kufanya upekuzi na kubaini uwepo wa vitu mbalimbali ikiwemo nebo za dawa 142” amesema Bw. Mtoro.

Amefafanua kuwa kukamatwa mtuhumiwa Mwangile kumetokana na kukamatwa kwa baadhi ya dawa ambazo tayari zimesambaza ambazo ni bandia, huku akieleza kuwa baadhi ya watuhumiwa ambao alikuwa anashirikiana tayari wanashikiliwa na Jeshi la Polisi.

“Dawa bandia ni uharibifu dhidi ya binadamu, ni unyama na ukatili kwani mtu akitumia dawa hizo anaweza kupoteza maisha” amesema Bw. Mtoro.

Ametoa wito kwa watanzania kuacha mara moja biashara haramu, kwani hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa wahusika wa vitendo hivyo.

Naye Mjumbe wa Shina namba sita Bi. Marry Mambo, ameishukuru TMDA kwa kufanikisha tukio la kukamatwa wa watuhumiwa huyo pamoja kushuudia upekuzi wa vitu ambayo vimekamatwa.

Amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa uongozi wa TMDA kwani kilichokuwa kinafanyika ni uharibifu wa mwili wa binadamu.

“Tunaomba adhabu kali ichukuliwe kwa wahusika kwani alichokuwa anafanya sio kitu kizuri katika jamii” amesema Bi. Mambo.

Previous articleUCHUMI WA TANZANIA WAPAA MIAKA MIWILI YA RAIS SAMIA-IMF
Next articleTFF YAPONGEZWA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA MICHEZO KIGAMBONI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here