AHUKUMIWA KUNYONGWA KWA KUMTEKA, KUMUUA MTOTO (08
NA JOSEA SINKALA, MBEYA
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya imemhukumu kunyongwa hadi kufa Musa Mbelechamo (32) Mkazi wa Bangwe Sumbawanga mkoani Rukwa, baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya kukusudia baada ya kumteka kisha kumuua mtoto wa miaka minane mwaka 2019.
Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Victoria Nongwa baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili na kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamuhuri juu ya mshtakiwa kutekeleza mauaji hayo makusudi akijua wazi kufanya hivyo ni kosa.
Jaji Nongwa amerejea kwa sehemu ushahidi wa jamuhuri ambao walikuwa na mashahidi saba akiwemo Baba mzazi wa marehemu, daktari aliyechunguza mwili wa mtoto baada ya kunyongwa pamoja na maafisa wa Polisi ambao kwa nyakati tofauti walieleza kupotea kwa mtoto Juniour Bakary ambapo alitafutwa bila mafanikio hadi alipopatikana akiwa amefariki dunia baada ya mtu huyo kukamatwa na kwenda kuonyesha alikotelekeza mwili wake katika eneo la Mlimanyoka baada ya kumteka kwa lengo la kuwalaghai wazazi wake wampatie fedha ili amwachie mtoto huyo.
Ushahidi huo wa upande wa Jamuhuri unaelezwa kutotikiswa kwa namna yoyote na upande wa utetezi ambao mshtakiwa akitoa utetezi wake chini ya kiapo hakuwa na maelezo ya kina kuhusu kesi inayomkabili zaidi ya kukana kutenda kosa hilo na kukiri kukamatwa mkoani Iringa wakati akiendelea na biashara zake.
Mwendesha mashtaka wa Serikali wakili Emmanuel Bashome aliiomba mahakama kutoa adhabu sawasawa na sheria inavyoelekeza ili iwe fundisho kwa jamii kwa ujumla hasa desturi ya baadhi ya watu kuendekeza tamaa kwa kufanya matukio maovu ikiwemo Ubakaji, ulawiti na mauaji ili kujipatia fedha na mauaji hayo anasema ni kinyume na kifungu namba 196 na 197 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.
Kwa mujibu wa hati ya Mashtaka, Mshtakiwa Musa Mbelechamo (32) mkazi wa Bangwe Sumbawanga mjini na kwa asili akitoka Nyamanolo Bungilo huko Ilemela mkoani Mwanza alikuwa akikabiliwa na kesi ya jinai namba 30/2021 ambapo inaelezwa mtu huyu akiwa kifungoni kwa kesi ya unajisi alisikiliza kupitia redio uwepo wa baadhi ya watu kuteka watoto na kuwataka wazazi au walezi wao kuwapatia fedha ili kumwaachia.
Inadaiwa kwamba baada ya kutoka gerezani kwa rufaa akiwa katika eneo la Sae Ilomba jijini Mbeya alikutana na mtoto Junior Bakary mwanafunzi wa darasa la pili kipindi hicho ambapo alitokomea naye hadi Mlimanyoka kisha kutafuta namba za simu za wazazi na kuwataka wampe Sh.Million kumi ili kumwachia mtoto wao hivyo katika harakati za kumtumia fedha mtoto alianza kupiga kelele baada ya kusikia sauti ya baba yake kwenye simu hivyo mshtakiwa kuamua kumziba pua na mdomo ili kutopiga kelele hali iliyomsababishia kukosa pumzi na baadaye kupoteza maisha.
Baada ya kugundua hilo mshtakiwa alikimbia kwa kwenda Makambako Njombe kisha mkoani Iringa ambapo uliandaliwa mtego na kumtumia fedha hizo hadi anapokamatwa katika eneo la Ipogolo mjini Iringa na baada ya kuhojiwa alikiri kumteka mtoto huyo ili apate fedha na akaenda na maofisa wa Polisi kuonyesha mahali alikotelekeza mwili wa mtoto Junior huko Mlimanyoka.
Jaji Victoria Nongwa ameeleza kuridhika na ushahidi huo bila kuacha shaka yoyote hivyo kumhukumu Musa Mbelechamo kunyongwa hadi kufa kwa kosa hilo la mauaji ya kukusudia ya mtoto wa miaka minne.