Home KITAIFA ADO SHAIBU: CCM ISIHODHI MCHAKATO WA KUPATIKANA KWA TUME HURU YA UCHAGUZI...

ADO SHAIBU: CCM ISIHODHI MCHAKATO WA KUPATIKANA KWA TUME HURU YA UCHAGUZI NA KATIBA MPYA

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ndugu Ado Shaibu amesema mchakato wa upatikanaji wa Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya unapaswa kuwa shirikishi, wazi na jumuishi.

Ndugu Ado ametoa kauli hiyo kwenye Mikutano Mikuu ya Majimbo ya ACT Wazalendo katika majimbo ya Kaliua na Urambo Mkoani Tabora aliyokuwa mgeni rasmi iliyofanyika tarehe 22 na 23 Juni 2023.

“Nimemsikia Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo hivi karibuni akisema mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya utasimamiwa na kuratibiwa na CCM. Hatutakubali hilo litokee. Hii si Katiba ya CCM, ni Katiba ya Watanzania, inapaswa kupatikana kwa mchakato wa wazi, jumuishi na shirikishi kwa makundi yote kwenye jamii” alisema Katibu Mkuu Ado Shaibu.

“Ni muhimu tujifunze kilichokwamisha mchakato wa Katiba Mpya mwaka 2014. Somo la kwanza ni kutanguliza mbele maslahi ya vyama dhidi ya maslahi ya Taifa. Ni muhimu vyama vyote vya siasa na makundi yote muhimu kwenye jamii yashirikishwe katika kujenga muafaka wa kitaifa ili tusikwame tena” alisisitiza Ado.

Pia, Ndugu Ado amerejea rai ya ACT Wazalendo ya kuandikwa upya kwa Sheria ya Uchaguzi ndani ya mwaka 2023 ili kuanzisha Tume Huru ya Uchaguzi itayosimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu ujao. Pia, Ndugu Ado ameitaka Serikali iweke wazi lini mchakato wa Katiba Mpya utaanza, hasa hatua muhimu za kupitiwa upya kwa sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Sheria ya kura ya maoni; kuitishwa kwa Mkutano wa Majadiliano ya Kitaifa kuhusu Katiba na kuundwa kwa Kamati ya Wataalam (Committee of Experts) ya kuchambua maoni ya wadau na kuandika Katiba Pendekezwa itayopigiwa kura ya maoni.

Baada ya ziara yake katika Mikoa ya Kigoma na Tabora, ziara ya Katibu Mkuu inaingia Mkoani Tanga (tarehe 25-28 Juni) ambapo Ndugu Ado atazungumza na viongozi wa Kata zote kwenye majimbo ya Tanga Mjini, Pangani na Mkinga kupitia Mikutano Mikuu ya Majimbo hayo.

Previous articleSEKTA YA MADINI KUONGEZA MCHANGO WAKE KWENYE PATO LA TAIFA MWAKA WA FEDHA 2023/24
Next articleUTAWALA BORA NA WA SHERIA NDIO MSINGI WA MAENDELEO YA UCHUMI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here