Home KITAIFA ACT WAZALENDO WATAKA HATUA ZA UWAJIBIKAJI UKATILI NA UNYANYASAJI WA ASKARI WA...

ACT WAZALENDO WATAKA HATUA ZA UWAJIBIKAJI UKATILI NA UNYANYASAJI WA ASKARI WA WANYAMAPORI DHIDI YA WAKULIMA MBARALI ZICHUKULIWE

 

Chama cha ACT Wazalendo kimepokea kwa masikitiko makubwa sana kuhusu tukio la ukatili na udhalilishaji lililofanywa na askari wa Wanyapori katika Kijiji cha Mwanawala Kata ya Imalilo, wilayani Mbarali, Mbeya.

 

Mnamo tarehe 10 Mei, 2023 askari wa wanyamapori wakitua na Hekopta katika Kijiji hicho na kuwashambulia wanakijiji jamii ya wafugaji na kusababisha mauaji wa mifugo (mbuzi na Mbwa wanne) kwa risasi za moto, kupora mifugo zaidi ya 250, udhalilishaji wa wanawake (kwa kuwavua nguo zao), kuwatesa kwa kuwachoma moto kwa kutumia mapanga na kuwapiga wananchi.

 

Kitendo hiki cha kikatili na kinachokiuka utu na haki za binadamu, kinatokana na mgogoro wa muda mrefu uliosababishwa na tangazo la Serikali Namba 28 la mwaka 2008, ambalo msingi wake ni kupanua eneo la Hifadhi ya Ruaha ili eneo la Bonde la Usangu lijumuishwe ndani yake.

 

Tangazo hili lililenga kuvifuta vijiji 28 vya Wilaya ya Mbarali, Mbeya ili kusudi eneo lake liingizwe kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo ilipandishwa hadhi kutoka pori la akiba mwaka 2006. Jambo lililopelekea kuongeza ukubwa wa eneo la hifadhi kwa kumega eneo la uzalishaji wa kilimo na ufugaji.Hatua ambayo ilipingwa kwa nguvu zote na wadau mbalimbali.

 

Aidha, tumeshangazwa kuona watendaji na askari wa TANAPA wanakiuka hadharani maamuzi ya Serikali ya Oktoba 25, 2022 kwa wananchi wa Mbarali kuviacha Vijiji 27 kikiwemo Kijiji cha Mwanawala visiondolewe na wananchi waendelee na shughuli zao. Uamuzi wa askari wa TANAPA na viongozi wa Kiserikali kubariki hatua hizi za kinyama msingi wake ni nini? Unalenga kumnufaisha nani?
Sambamba na hilo, matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu unanofanywa na Askari wa Hifadhi ya Taifa (TANAPA) yamekuwa yakijirudia rudia hususani maeneo yenye migogoro. ACT Wazalendo inapinga vikali hatua za matumizi ya nguvu na ukatili dhidi ya wananchi.

Tumemsikia Waziri Mkuu Ndugu Kassim Majaliwa ameagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda Mbarali kuongea na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali kuhusu Swala hilo, na amekiri kwamba hatua hiyo imefanywa kinyume na maamuzi ya Serikali ya kuwaacha wananchi kwenye Vijiji 27 vya GN28 kikiwemo cha Mwanawala.

 

Pamoja na maagizo haya, ACT Wazalendo hatuoni  maagizo yaliyotolewa yakileta matunda katika kushughulikia migogoro ya wananchi na mamlaka za hifadhi na kwa suala hili Mahususi la uvunjifu wa haki za binadamu, Mbarali. Hivyo basi, tunaitaka hatua zifuatazo zichukuliwe kwa haraka zaidi…..

 

Serikali isitishe zoezi la kuwahamisha wananchi hao badala yake itumie njia shirikishi za kuhakikisha utunzaji wa mazingira na kilimo chenye kuendeleza uhifadhi. Wananchi washirikishwe kwenye kutafsiri mipaka, kuweka alama na kukamilisha malipo ya fidia kwa wale watakaonekana kuvuka mipaka ya awali mwaka 2001.

 

Serikali isaidie kuimarisha na kuboresha mifumo ya kilimo cha umwagiliaji wa kisasa ili kuhakikisha kilimo kinaendelea na mazingira yanahifadhiwa.

 

Serikali kuwahudumia kwa Matibabu na kuwalipa fidia Stahiki Wanawake waliochomwa kwa Moto na Kijana aliyelazwa hospitali kwa kupigwa na Maafisa wa TANAPA.

 

TANAPA warudishe Mifugo Zaidi ya 250 waliyonyag’anya Wafugaji na walipe Gharama ya Mbuzi wawili na Mbwa mmoja waliowaua kwa Risasi za Moto.

 

Maafisa wa TANAPA waliotekeleza kitendo hicho wafutwe kazi na kufunguliwa mashtaka ya Jinai wafikishwe mahakamani, Kwani wamekiuka haki za Binadamu.

 

Kwa sasa hoja za upanuzi wa maeneo ya hifadhi na kupandishwa kwa hadhi kwa maeneo hayo, zimekuwa zikiongeza kasi ya migogoro ya ardhi kwa kuwa yanamega maeneo yanayotumiwa na wananchi kwa ajili uzalishaji, makazi au shughuli za kijamii. Migogoro ya ardhi kati ya wananchi (jamii) na Serikali kupitia taasisi zake, uchukuaji wa maeneo kwa jina la hifadhi, rachi ya taifa, vyombo vya ulinzi na usalama (Jeshi la wananchi na Magereza) Serikali imekuwa inachochea na kuzalisha migogoro na mauaji. Ni muhimu sana kuzingatia mahitaji ya kijamii kuliko hoja zingine.

 

Imetolewa na;

Ndugu Anthony Ishika.

Naibu Waziri Kivuli Maliasili na Utalii,
ACT Wazalendo.
12 Mei, 2023.

Previous articleMILIONI 214 ZAWEKEZWA NA SERIKALI KUBORESHA MIUNDOMBINU YA MAPOROMOKO YA ULUGURU
Next articleNCHI YA VITANDA VITUPU, MBWA WACHUKUA NAFASI YA WATOTO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here