Na Mwandishi Wetu Kilwa Kivinje-Lindi
Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya Chama cha ACT Wazalendo, Abdul Nondo amesema ni miezi sita sasa imepita tangu serikali imalize mkataba wake na kampuni ya kuhudumia makontena ya TICTS mwezi Novemba 2022, kutokana na kilichoelezwa ni ufanisi mdogo wa uendeshaji wa magati kadhaa katika bandari ya Dar es Salaam ambapo walitarajia wawekwe wazi kwamba anayefanya kazi baada ya TICTS bandarini ni nani na kwa utaratibu gani alipewa kazi hiyo na anafanya kazi gani.
Amesema hayo leo Julai 02, 2023 wakati akihutubia wananchi wa Kilwa Kivinje mkoani Lindi ambapo Nondo amedai kuwa, kwa taarifa ambazo kama chama walio nazo sasa ni kwamba kazi ambayo alikuwa amepewa TICS (Under Hutchison Port Holding) ya uendeshaji (Operation ) na ukusanyaji wa fedha katika Bandari ya Dar es Salaam sasa hivi inafanywa na kampuni ya Adani Group chini ya familia ya Gautam Adani & Rajeshi Adani.
Nondo ameongeza kuwa, kupitia mtandao wa club house hapo jana Julai Mosi, mwaka huu alimuuliza swali Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali kuhusu kampuni ya Adani kufanya kazi alizokuwa akifanya TICTS ambapo alijibu kuwa,
kazi zilizokuwa zikifanywa na TICTS kwa sasa sasa zinafanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na wala Adani Group hayupo .
Kufuatia hilo Nondo ametoa rai kwa serikali kwa kusema
“Moja ya jambo ambalo serikali inapaswa kujiepusha nalo mara zote ni kuficha mambo ambayo baadaye yakishafahamika na umma yanazua mjadala na serikali kutumia nguvu kubwa kutetea na kusafisha . Haya ni mambo ambayo yanahusu maslahi ya nchi na ufanisi wa kazi inayofanywa katika maeneo kadhaa bandarini ukilinganisha na kampuni iliyopewa kazi ya operesheni hivi sasa na utaratibu uliotumika kutoa hiyo kazi ya operesheni”
Nondo ameendelea kwa kusema kuwa, taarifa ambazo wanazo hivi sasa ni kwamba TPA sasa hivi inafanya kazi moja tuu ya kukusanya mapato lakini kazi zote za operesheni na uendeshaji zinafanywa na kampuni inayoitwa Adani Group, na kusisitiza kuwa kampuni hiyo ni ya kidalali, haina wafanyakazi wala haina mitambo.
“kampuni hii inatumia mitambo ya TICTS kufanya kazi na inamlipa TICTS fedha kwa yenyewe kutumia mitambo ya TICTS ,kampuni hii haina wafanyakazi (ManPower ) inatumia wafanyakazi waliokuwa wanafanya kazi chini ya TICTS. Kampuni hii inalipwa na TPA fedha nyingi kwa ajili ya hiyo operesheni, operesheni hizo ni zipi?.Ikiwa kampuni haina vifaa wala wafanyakazi inalipwa kwa kazi gani?” alihoji Nondo
Vilevile ameeleza kuwa TICTS ilisumbua kutokana na ufanisi wake mdogo wa ufanyaji kazi na hivyo ikawalazimu kalupiga kelele na kutaka isiongezewe mkataba, ambapo amehoji kampuni ya Adani Group inavyodaiwa kufanya kazi bandarini imeleta ufanisi gani kwa miezi tangu imeanza kufanya kazi.
Aidha, Nondo amehoji utaratibu wa kumpata Adani Group ili kufanya kazi ya operesheni katika maeneo ambayo TICS walikuwa wanafanya kazi?
“Tenda (Competitive bidding) ya kumpata Adani Group kufanya operesheni ilitangazwa lini? ,walioshindanishwa hadi kumpata Adani Group ni kampuni gani? . Adani Group anafanya kazi ya operesheni kwa muda gani na kwa makubaliano gani?, kwanini serikali imeficha kuambia umma kuhusu kampuni inayofanya kazi ya operesheni baada ya TICS kumaliza mkataba wake?.
Hata hivyo ameishauri serikali kwa kusema kuwa, ni vyema masuala kama hayo, serikali iwe inatoa taarifa na kuweka wazi kuliko kuficha, sababu kuficha ficha ndiyo chanzo cha rushwa na ufisadi, na kusisitiza kuwa majibu ya serikali katika jambo hilo ni muhimu ili watanzania wajue.
“Tuliokuwa tunapiga kelele juu ya ufanisi mbovu wa TICTS tulitarajia kuambiwa na serikali kwa uwazi juu ya ufanisi wa kampuni inayofanya kazi sasa baada ya TICTS na kujua makubaliano ya serikali na kampuni hiyo Adani Group ni makubaliano ya namna gani, na kwanini Adani Group anafanya kazi ya Operation kwa vifaa vya TICTS ikiwa tulisema awali vifaa vya TICTS na mitambo havina ufanisi ,huyu Adani Group analipwa na TPA kwa kazi gani hasa anayoifanya ikiwa hana vifaa wala wafanyakazi?” alisisitiza
Nondo amehitimisha kwa kueleleza kuwa, wao kama chama wanahoji kwa upendo wa dhati na kwa maslahi ya nchi ili rasilimali za Taifa ziweze kunufaishaTaifa na kupelekea dhamira ya dhati ya kuleta maendeleo kwa wananchi itimie kupitia manufaa ya rasilimali zetu.